Monday, May 21, 2012

JACK, KABULA WASHINDWA KUMUAGA MAFISANGO


 Jacqueline Pentzel ‘Jack Chuz’.

Miriam Jolwa ‘Jini Kabula’.
Stori: Erick Evarist
WAIGIZAJI masistaduu wa filamu za Kibongo, Jacqueline Pentzel ‘Jack Chuz’ na Miriam Jolwa ‘Jini Kabula’, Ijumaa iliyopita walishindwa kuaga mwili wa kiungo mshambulia wa Timu ya Simba, marehemu Patrick Mafisango kwenye Viwanja vya TTC Chang’ombe, Dar kutokana na umati mkubwa uliojitokeza.
Huku wakijinadi kuwa ni mashabiki wa kufa wa soka Bongo, wakiwa eneo hilo, mastaa hao waliliambia Ijumaa Wikienda kuwa walijisikia vibaya kushindwa kupata nafasi ya kumwona kwa mara ya mwisho marehemu Mafisango.
“Imetuuma sana, wametangaza muda wa kuaga umekwisha na sisi hatujapata nafasi ya kufika kwenye jeneza. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi,” alisema Jack.
Mafisango (32) alifikwa na mauti kwa ajali ya gari iliyotokea eneo la Chuo cha Ufundi cha Veta, Dar na alitarajiwa kuzikwa wikiendi iliyopita nyumbani kwao Kinshasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.